Serikali imeweka sheria kali za kuwalinda Wakenya wanaofanya kazi ughaibuni dhidi ya kudhulumiwa na waajiri.
Kulingana na Katibu katika Wizara ya Leba na Ukuzaji Maarifa Shadrack Mwadime, serikali imesaini mwafaka na mataifa kadhaa utakaohakikisha wafanyakazi wa kenya hawadhulumiwi ughaibuni.
Amesema mwafaka huo unaambatana na sheria za Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi (ILO).
Aidha, ameongeza kuwa serikali itatuma afisa mmoja kwa kila nchi ili kuhakisha haki za Wakenya wanaofanya kazi katika mataifa ya kigeni hazikiukwi.
Serikali pia imeamrisha Balozi za Kenya kuwasiliana na Wakenya wanaofanya kazi katika mataifa yao.
Katibu Mwadime alisema hayo jana Alhamisi jioni katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), aliposhuhudia kundi la vijana 16 wa Kenya waliosafiri kwenda kufanya kazi nchini Oman.
Sheria hizo zinafuatia ripoti kadhaa kuhusu Wakenya wanaodhulumiwa na waajiri wao ughaibuni hususan katika mataifa ya Mashariki ya Kati.