Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imemuamuru Kassim Abdi Sebu, anayehusishwa na ghasia zilizoshuhudiwa katika Kaunti ya Homa Bay Jumapili, Agosti 16, 2026, kuripoti katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI ya kaunti hiyo kwa mahojiano.
Agizo hilo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu ghasia zilizotokea wakati wa shughuli mbalimbali katika kaunti hiyo.
Huko Kisumu, washukiwa 15 waliokamatwa wakiwa na silaha kabla ya mkutano wa hadhara walifikishwa mahakamani ambapo DCI ilipatiwa siku nne za kufanya uchunguzi zaidi kuhusu suala hilo.
Polisi pia walisema Oliver Jaoko, anayejulikana kwa jina la Olivetti, ambaye anadaiwa kuhusishwa na washukiwa hao 15, ameagizwa kuripoti katika Makao Makuu ya DCI ya Mkoa, Kisumu.
Hii ni baada ya Olivetti kujiwasilisha kwenye makao makuu ya DCI Nairobi awali akiwa na mbunge Babu Owino na Gavana James Orengo kati ya wengine, lakini hawakupokelewa.
Huko oma Bay, washukiwa 12 walifikishwa mahakamani na kupatiwa masharti mbalimbali ya dhamana.
Washukiwa wengine wawili wanachunguzwa kuhusiana na visa vya kutumia bunduki na watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.
NPS imejitolea kuendelea kufuatilia watu wanaohusika na ghasia za magenge na uhalifu mwingine, huku ikiahidi kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Huduma hiyo pia imewashukuru wananchi kwa kuunga mkono juhudi za polisi za kurejesha usalama.