Wawakilishi wa Kenya katika kitengo cha soka ya wavulana ya mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili yanayoendelea mjini Morogoro nchini Tanzania – Kakamega na Yala, hii leo Jumanne wameyaaga mashindano hayo baada ya matokeo mseto.
Kakamega almaarufu Green Commandoes, ambao ni mabingwa wa kitaifa mwaka huu walikabwa koo na Bukedea ya Uganda bao moja kwa moja. Awali, Kakamega walishindwa mchuano wa kwanza na pili wa makundi.
Nao Yala walio wa pili nchini, walilazwa bao moja kwa nunge na CGF Kigali ya taifa la Rwanda.
Kwenye mchuano wa ufunguzi, Yala waliadhibiwa na St. Mary’s Kitende ya Uganda kisha wakapata sare kwenye mchuano wa pili dhidi ya shule ya upili ya Morogoro.
Taarifa ya Boniface Mutsotso