Mwimbaji wa nyimbo za Injili na Balozi wa Nia Njema wa UNHCR, Mercy Masika, amezitaka mamlaka kusawazisha utekelezaji wa sheria na huruma.
Ombi lake linafuatia agizo la Rais William Ruto la kuzuia wageni kufanya biashara rejareja jijini Nairobi.
Masika ametambua umuhimu wa kuwa na maeneo ya umma yaliyo salama, yenye utaratibu na yanayosimamiwa ipasavyo, lakini akaonya dhidi ya hatua za utekelezaji wa sheria zinazoweza kudhoofisha utu wa wakimbizi na watu wengine waliolazimika kuyahama makazi yao.
Katika taarifa yake, mwanamuziki huyo alisema wakimbizi wengi hutegemea biashara zisizo rasmi ili kuzikimu familia zao na kujenga upya maisha yao, hasa kutokana na vikwazo wanavyokumbana navyo katika kupata ajira rasmi.
Aliwasifu wakimbizi kama zaidi ya wanufaika wa misaada ya kibinadamu, akisema pia ni wazazi, wajasiriamali, wafanyakazi na wachangiaji katika jamii wanamoishi.
Masika amependekeza suluhu za vitendo zitakazowasaidia wakimbizi walioathiriwa kufuata sheria, zikiwemo kutengewa maeneo maalumu ya masoko, fursa halali za ajira na mipango ya kukuza ujuzi.
Pia ameitaka serikali ya kitaifa na zile za kaunti kushirikiana na mashirika ya kibinadamu, asasi za kiraia na wawakilishi wa wakimbizi kutafuta suluhu zinazolinda utaratibu wa umma pamoja na utu wa kila mtu.
Kauli yake inajiri huku mjadala kuhusu uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni katika uchumi usio rasmi wa Nairobi ukizidi kushika kasi.