Bei ya mafuta ilipanda na kuvuka dola 100 (£74) kwa pipa siku ya Jumatano kufuatia mashambulizi mapya katika mzozo unaoendelea kati ya Marekani na Iran, pamoja na mashambulizi ya Wahouthi nchini Saudi Arabia.
Katika mashambulizi ya kulipizana kisasi, Marekani ilishambulia meli tano za kubeba mafuta za Iran baada ya Tehran kulenga moja ya manowari zake.
Mafuta ghafi ya Brent, ambayo hutumika kama kipimo kikuu cha bei za mafuta duniani, hayajafikia kiwango hicho tangu mwishoni mwa Julai, wakati makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya Iran na Marekani yalipovunjika.
Kundi la Wahouthi la Yemen, linaloungwa mkono na Iran, pia lilishambulia miundombinu ya mafuta nchini Saudi Arabia siku ya Jumanne, huku likiendelea kulenga meli za mafuta zinazopita katika Bahari ya Shamu.
Ingawa bei ya Brent ilishuka baadaye hadi dola 99.90 kwa pipa, wachambuzi wanaonya kuwa ongezeko lolote la mvutano katika Mashariki ya Kati linaweza kusababisha bei hizo kupanda tena.
Mashambulizi ya Marekani dhidi ya meli hizo tano za Iran yalihusisha meli nne zilizokuwa katika Ghuba ya Oman na zinazohusishwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), pamoja na meli nyingine iliyokuwa karibu na Kisiwa cha Kharg.
Iran ilijibu kwa kurusha makombora kuelekea kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan, huku mengi yakidunguliwa. Tehran pia ilisema ilizishambulia meli mbili za Marekani na meli nane za mafuta katika Mlango wa Hormuz.
Wahouthi na Saudi Arabia wamekuwa wakishambuliana tangu Julai baada ya makubaliano yao yasiyo rasmi ya kusitisha mapigano kusambaratika.
Taarifa ya BBC