Wetang’ula awataka wanawake kuwania nafasi za kisiasa uchaguzi wa 2027

Alimtaja Mwakilishi wa Wadi ya Sitikho, Grace Sundukwa, kama mfano wa kuigwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amehimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi Mkuu wa 2027, badala ya kujikita katika kuwaunga mkono wanasiasa wa kiume.

Akizungumza leo kwenye mkutano na viongozi wanawake kutoka wadi nne za eneo bunge la Kimilili katika makazi yake Kabuchai, Wetang’ula alisema ushiriki mkubwa wa wanawake katika siasa ni muhimu ili kuongeza uwakilishi wao katika maamuzi ya kaunti na kitaifa.

“Wanawake hawafai kuwa wapiga kura na wafuasi wa malengo ya kisiasa ya watu wengine pekee. Nataka kuona wanawake wengi wakijitokeza, kuwania nafasi za uongozi na kushindana katika ngazi zote,” alisema.

Wetang’ula alimtaja Mwakilishi wa Wadi ya Sitikho, Grace Sundukwa, kama mfano wa kuigwa, akisema amefanikiwa kushinda kiti hicho mara tatu.

Aliwahimiza wanawake kujifunza kutokana na mafanikio yake na kuwania nyadhifa za kuchaguliwa badala ya kusubiri kuteuliwa.

Pia aliwahimiza vijana na wanawake kujisajili kama wapiga kura, akisema ushiriki wao utasaidia kuamua mwelekeo wa kisiasa wa nchi.

Spika huyo aliwataka wakazi wa Magharibi mwa Kenya kuendelea kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza, akitaja uwekezaji katika elimu na miundombinu, ikiwemo vyuo vya kitaifa vya polytechnic vya Kisiwa, Sang’alo na Matili.

Wetang’ula alisema eneo hilo lazima lifanye maamuzi ya kimkakati baada ya 2027, akisisitiza kuwa umoja, mipango na ushirikiano vitakuwa muhimu katika kulinda maslahi ya Magharibi mwa Kenya na kuimarisha nafasi yake katika uongozi wa kitaifa.

Share This Article