Uganda yakomesha ushiriki michezo ya Invictus

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba alisema Uganda haitaki kuonekana kupinga utawala wa Mfalme wa Uingereza.

Marion Bosire
2 Min Read
Muhoozi Kainerugaba - Mkuu wa Majeshi ya Uganda

Taifa la Afrika Mashariki la Uganda limejiondoa katika Michezo ya Invictus, likisema halitashiriki tena katika mashindano hayo yanayohusishwa na Mwanamfalme Harry.

Hii ni baada ya mvutano kuripotiwa kuzidi kati ya Mwana huyo wa mfalme na baba yake, Mfalme Charles III.

Kupitia kitandazi cha X, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alitangaza uamuzi huo akisema Uganda haitaki kuonekana kuwa inapinga utawala wa Mfalme wa Uingereza, ambaye alimtaja kuwa kiongozi anayeheshimiwa sana.

“Kwa kutotaka kutafsiriwa kuwa tunampinga Mtukufu Mfalme Charles III wa Uingereza, ambaye tunamheshimu sana, Uganda imejiondoa katika Michezo ya Invictus. Hatutashiriki katika jambo lolote ambalo halijaidhinishwa na Mtukufu Mfalme,” Muhoozi aliandika.

Michezo ya Invictus ni mashindano ya kimataifa ya michezo kwa wanajeshi na wanajeshi wa zamani ambao wamejeruhiwa, kupata madhara au kuugua kutokana na huduma zao.

Yalianzishwa na Mwanamfalme Harry, mwaka 2014, akichochewa na uzoefu wake wa kutumikia katika Jeshi la Uingereza na kazi yake ya kusaidia wanajeshi waliojeruhiwa.

Yeye na mke wake Megan Markle walihamia Uingereza hivi maajuzi kutoka Marekani ambako wameishi kwa muda.

Siku chache baada ya kurejea, Mfalme Charles alitoa tamko rasmi akisisitiza kwamba bado Harry na mkewe sio wanafamilia wa familia ya ufalme wanaofanya kazi, hatua iliyochukuliwa na wengi kuwa ishara ya mvutano kati ya baba na mwana.

Share This Article