Baraza la Magavana Nchini, CoG na Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi na Wakunga wa Kenya, KNUNM hatimaye wameafikia makubaliano.
Baada ya mkutano wa leo wametia saini makubaliano muhimu ya kurejea kazini, na hivyo kumaliza mgomo wa wauguzi uliodumu kwa siku 41 nchini kote.
Mgomo huo, ulioanza Julai 29, ulikuwa umeathiri huduma za afya katika hospitali za umma katika kaunti zote 47.
Baada ya mazungumzo ya siku nzima yaliyofanyika kwa faragha, Katibu Mkuu wa KNUNM, Seth Panyako, ametangaza kusitishwa kwa mgomo huo mara moja na kuwaagiza wanachama wote kurejea vituoni mwao ndani ya saa 24.
Makubaliano hayo yanashughulikia malalamiko ya muda mrefu kuhusu maslahi ya wauguzi pamoja na utekelezaji wa mfumo wa Makubaliano ya Kurejea Kazini wa mwaka 2017.
Chini ya makubaliano hayo mapya, wauguzi watapata nyongeza ya shilingi elfu 8 katika marupurupu yao ya hatari katika maeneo ya kazi pamoja na nyongeza ya shilingi elfu 5 katika marupurupu ya sare, sawa na ongezeko la jumla la shilingi 13,000 katika marupurupu yao.
Makubaliano hayo yamezuia sekta ya afya ya umma nchini kusambaratika zaidi, huku Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno Kenya, KMPDU ukiwa umetishia kujiunga na mgomo huo kutokana na uchovu wa kiwango cha juu miongoni mwa madaktari.
Huduma za kawaida katika vituo vya afya vya umma na hospitali za rufaa zinatarajiwa kurejea kikamilifu kesho.