Msanii wa muziki wa Kenya Samidoh amewataka Wakenya kuthamini ubinadamu na kukataa ubaguzi unaotokana na utaifa, akisema Waafrika wanapaswa kuweka ubinadamu mbele ya mipaka ya kitaifa.
Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, msanii huyo aliwakumbusha Wakenya kuwa tofauti za lafudhi au utaifa hazimfanyi mtu kuwa binadamu wa kiwango cha chini.
“Lafudhi tofauti haimfanyi mtu kuwa binadamu wa kiwango cha chini. Utaifa tofauti haufanyi machozi ya mtu mwingine yasiwe na uchungu,” alisema Samidoh.
Pia alikosoa kile alichokiita viwango viwili kinzani nchini Kenya, akihoji kwa nini baadhi ya Wakenya huwafukuza raia wa kigeni wanaojishughulisha na biashara ndogo huku wakipuuza ufisadi unaohusisha watu wanaotuhumiwa kuiba mabilioni ya fedha za umma.
“Kenya imekuwa ikijulikana kwa ukarimu,” alisema, kabla ya kuonyesha kile alichokitaja kuwa kinzani katika namna jamii inavyoshughulikia makosa.
Samidoh alitoa mfano wa Mburundi anayekimbizwa kwa kuuza njugu karanga huku afisa mkuu anayetuhumiwa kuiba mabilioni akiachwa.
“Huo si uzalendo, huo ni ujinga!” alisema.
Msanii huyo aliwataka Wakenya kufanya vizuri zaidi na kuwatendea Waafrika wenzao kwa heshima na utu.
Ushauri wa mwaniaji huyo wa ubunge wa eneo la Ol Joro Orok unafuatia visa vilivyoripotiwa vya raia wa Kenya kushambulia wageni wanaofanya biashara nchini, kufuatia maelekezo ya serikali kuhusu namna wageni wanapaswa kutekeleza shughuli nchini.