Miss World Tanzania kuvishwa taji na Miss World

Fainali ya mashindano ya Miss World Tanzania itaandaliwa leo usiku katika ukumbi wa Super Dome huko Masaki, jijini Dar es Salaam.

Marion Bosire
2 Min Read
Miss World Ethiopia na Miss World wakiwasili Tanzania

Mshikilizi wa sasa wa taji ya mashindano ya ulimbwende duniani Miss World, Opal Suchaata raia wa Thailand yuko nchini Tanzania ambapo alialikwa na waandalizi wa mashindano ya Miss World Tanzania.

Aliwasili Tanzania Aprili 16, 2026 ambapo alipokelewa katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na Mustafa Hassanali, mkurugenzi wa mashindano ya Miss World Tanzania.

Tayari amefika katika kambi ya wanaoshindania taji hiyo ya urembo ya Tanzania na kutagusana nao huku akiwapa mawaidha mbali mbali.

Opal atahusishwa katika kuvisha mshindi wa mashindano hayo ya Tanzania taji, katika fainali leo usiku katika ukumbi wa Super Dome, mashindano yatakayoonyeshwa moja kwa moja na ITV na kwenye chaneli ya Miss World Tanzania kwenye YouTube.

Akizungumzia maandalizi ya fainali Hassanali alisema mashindano ya mwaka huu yamebeba historia ya kipekee, ambapo kwa mara ya kwanza mshindi atavishwa taji na mrembo huyo wa dunia, hali itakayoinua hadhi ya mashindano hayo na kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa.

Mashindano hayo ya urembo mwaka huu yamevutia washindani 20 watakaoonyesha weledi wao usiku wa leo ambapo majaji wanajumuisha, Mwajuma Hamza, Issa Muhidin Michuzi, Mbiki Msumi, Sebastian Kolowa, Rita Paulsen, Hussein Hamadi na Doris Mollel.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda anatarajiwa kuhudhuria hafla ya leo kama mgeni rasmi, waandalizi wakitaja uwepo wake kuwa muhimu kwa usiku wa kusherehekea urembo, kusudi na nguvu ya utamaduni na sanaa.

Makonda awali alikuwa amewataka waandaaji wa mashindano ya urembo nchini Tanzania kutolumbana, kulipotokea mkanganyiko kati ya mashindano ya Miss World Tanzania na Miss Tanzania.

Atakayetwaa taji usiku wa leo, ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya urembo yaani Miss World, mwezi Septemba mwaka huu nchini Vietnam.

Share This Article