Baraza la Mawaziri nchini Uganda limeidhinisha hatua ya serikali kuchukua usimamizi wa chuo kikuu cha Busoga na kukiendesha kama chuo kikuu cha umma, huku kikibadilishwa jina na kuitwa “Iganga University”.
Chuo hicho kitakuwa chuo kikuu cha kwanza cha umma katika eneo zima la Busoga.
Hatua hiyo inasogeza karibu kukamilika kwa mpango wa serikali wa muda mrefu wa kukichukua chuo hicho, ingawa bado Bunge linapaswa kuidhinisha kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho kipya.
Waziri wa ICT na Mwongozo wa Kitaifa nchini Uganda, Justine Kasule Lumumba, alitangaza uamuzi huo leo Jumanne, kufuatia kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Jumatatu, Oktoba 5, 2026.
Lumumba alisema Baraza la Mawaziri lilijadili pendekezo la kuanzisha taasisi hiyo ya elimu ya juu ya Busoga kama chuo kikuu cha umma na kuamua kukipa jina la Iganga University.
Serikali imetenga Shilingi za Uganda bilioni 89.998 kwa ajili ya mpango huo, fedha zinazolenga kusaidia maendeleo ya eneo la Busoga kupitia taasisi hiyo ya elimu ya juu.
Chuo kikuu cha Busoga ni chuo cha kibinafsi kilichoanzishwa mwaka 1998/99 na Dayosisi ya Busoga ya Church of Uganda.