KMPDU yataka hatua za haraka kukabiliana na Ebola

Inaihimiza serikali kulinda wahudumu wa afya ambao huenda walitangamana na mgonjwa wa kwanza aliyefariki.

Marion Bosire
2 Min Read
Dkt. Davji Bhimji Atellah, atibu Mkuu KMPDU

Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini, KMPDU, kimetaka hatua za haraka zichukuliwe kufuatia kuthibitishwa kwa kisa cha ugonjwa wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo nchini na kifo cha mgonjwa huyo.

Katika taarifa iliyotolewa mnamo Oktoba 6, 2026, Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Bhimji Atellah alituma rambirambi kwa familia ya marehemu huku akipongeza wahudumu wa afya waliohudumia mgonjwa huyo licha ya hatari zilizokuwepo.

Chama hicho kinaihimiza serikali kuwalinda mara moja wahudumu wa afya ambao huenda walitangamana na mgonjwa huyo kupitia uchunguzi wa kimatibabu, usaidizi wa kisaikolojia na ufuatiliaji unaofaa.

KMPDU pia inataka pia vituo vyote vya afya kuwa na vifaa maalum vya kujikinga, miongozo ya kuzuia maambukizi na mafunzo ya kutosha ili kudhibiti visa vinavyoshukiwa vya Ebola kwa usalama.

Aidha, chama hicho kinataka kuwepo kwa ufuatiliaji wa uwazi na madhubuti wa watu waliotangamana na mgonjwa (contact tracing), kikionya kwamba upungufu wa habari unaweza kuchochea hofu na uvumi.

Pia kinahimiza serikali kuthibitisha kuwa maeneo ya kutenga wagonjwa na vituo vya matibabu ya magonjwa ya kuambukiza yenye madhara makubwa vinafanya kazi, vina vifaa stahiki na vina wafanyakazi waliofunzwa.

KMPDU ilisema wahudumu wa afya na vyama vyao lazima washirikishwe katika miundo ya kitaifa na ya kaunti ya kukabiliana na dharura, ikisisitiza kwamba kulinda wafanyakazi wa mstari wa mbele ni muhimu katika kuilinda nchi.

Share This Article