Rais William Ruto ameiagiza Kamati ya Baraza la Usalama wa Kitaifa (NSCC) kukutana na kutathmini hali ilivyo baada ya kufariki kwa mgonjwa aliyeambukizwa ugonjwa wa Ebola.
Kifo cha mgonjwa huyo, Mkenya aliyeishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa kipindi cha miaka 7 na ambaye alirejea nchini Jumamosi iliyopita, ni kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kuripotiwa nchini.
Kwenye taarifa, Ruto pia ameiagiza NSCC kupendekeza hatua zinazofaa za kuilinda nchi dhidi ya msambao zaidi wa ugonjwa huo huku akitaka hatua madhubuti kuchukuliwa kukabiliana nao.
Serikali imeimarisha uangalizi wa watu waliotangamana na mgonjwa huyo ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola nchini.
Waliowekwa kwenye karantini ni jamaa wanane wa marehemu ambao dalili zao zinafuatiliwa kwa karibu kila siku.
Wengine waliowekwa kwenye karantini ni wahudumu 21 wa afya waliomshughulikia mgonjwa huyo alipokimbizwa katika hospitali moja jijini Nairobi kwa matibabu punde baada ya kurejea nchini.
Hadi kufikia sasa, abiria wapatao 27 waliosafiri na marehemu kwenye ndege kutoka jijini Kampala nchini Uganda wametambuliwa na mawasiliano nao kufanywa huku hatua mwafaka za afya ya umma zikichukuliwa na mamlaka.
Serikali inasema timu zake za uangalizi na kupambana na ugonjwa huo ziko macho kuhakikisha hakuna msambao wa ugonjwa wa Ebola utatokea nchini kote.
Ugonjwa huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,000 nchini DRC huku wengine zaidi ya 8,000 wakiambukizwa.
Umoja wa Mataifa, UN unaonya kwamba mlipuko huo, unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo, ndio unaoenea kwa kasi zaidi kuwahi kuripotiwa katika histioria.