Murkomen: Serikali itakabiliana na wanaovuruga maandamano ya amani

Murkomen aliwataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za kawaida siku ya Alhamisi, wanafunzi wakitakiwa kuhudhuria masomo shuleni.

Tom Mathinji
1 Min Read
Kipchumba Murkomen - Waziri wa Usalama wa Taifa.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ameonya kuwa serikali itakuchua hatua za kisheria dhidi ya mtu au kundi lolote litakalovuruga maandamano ya amani kwa kuzua vurugu, uporaji, uharibifu wa mali, kutatiza biashara au kuhusika katika aina yoyote ya uhalifu.

Akizungumza Jumatano jioni, Murkomen alihakikisha kuwa maafisa wa usalama watawalinda Wakenya wanaodumisha amani na wanaotekeleza shughuli zao za kawaida.

Alisema maafisa wa polisi wako tayari kuwalinda na kuwaelekeza waandamanaji siku ya Alhamisi, akiwasihi kuzingatia sheria kikamilifu na kutobeba silaha zozote.

“Tunawahimiza waandalizi na washiriki wa maandamano hayo kuzingatia sheria wakati wa maandamano hayo,” alisema Murkomen.

Wakati huo huo, Waziri huyo aliwataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za kawaida siku ya Alhamisi, wanafunzi wakitakiwa kuhudhuria masomo shuleni.

Hata hivyo Murkomen alidai kwamba baadhi ya wanasiasa wanalenga kuvuruga maandamano hayo kwa kutumia makundi ya wahalifu ili kuzua fujo, kulenga biashara na kushambulia wananchi.

“Tunafuatilia habari za kijasusi kuhusu baadhi ya wanasiasa wanaopanga kuwatumia wahuni kuvuruga maandamano ya amani ya Alhamisi, watakamatwa na kuzuiliwa,” alisema Murkomen.

Maandamano yanatarajiwa kuandaliwa siku ya Alhamisi, kuwakumbuka waliofariki kwenye maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha mwaka 2024.

Share This Article