Subira ya miaka minne hatimaye imekamilika huku zikisalia saa za kuhesabu, kabla ya kuanza kwa pata shika ya Kombe la Dunia makala ya 23 leo Alhamisi.
Wenyeji wenza Mexico watashuka uwanjani Mexico City kuanzia saa nne usiku dhidi ya Bafana Bafana ya Afrika Kusini katika pambano la kundi A.
Itakuwa mechi ya tano ya ufunguzi ya Kombe la Dunia, Mexico wakishinda 2, kutoka sare mchuano mmoja na sare mbili, Afrika Kusini walipokuwa wenyeji mwaka 2010 timu hizo zikitoka sare ya bao moja.
Mexico almaarufu El Tri, wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya 18 mwaka huu, huku wakijivunia kucheza hadi robo fainali mara mbili mwaka 1970 na 1986.
Bafana Bafana nao watakuwa wakishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya nne; ikiwa mwaka 1998, 2002, 2010, ingawa hawajawahi kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

Mchuano huo utatanguliwa na sherehe zikiongozwa na wasanii tajika wakiwemo Shakira na Burna Boy watakaoporomosha kibao chao rasmi cha Kombe la Dunia cha Dai Dai.
Wasanii wengine watakaoporomosha muziki leo ni Alejandro Fernandez, Belinda, Danny Ocean, J Balvin, Lila Downs, Los Angeles Azules, Mana na Tyla.

Sherehe ya ufunguzi itaanza dakika 90 kabla ya kung’oa nanga kwa mechi ya ufunguzi.
Mataifa mengine yanayoandaa fainali hizo pia yatakuwa na sherehe za ufunguzi sawia na za leo kabla ya mechi ya ufunguzi.