Kongamano la Bara kuhusu Vijana, Amani, Usalama na Wanawake kukamilika kesho

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maji, Amani na Uongozi Shirikishi barani Afrika” .

Marion Bosire
2 Min Read
Rais Evariste Ndayishimiye akifungua rasmi mkutano wa bara hili kuhusu vijana na wanawake

Awamu ya 5 ya kongamano la Bara hili kuhusu Vijana, Aman na, Usalama, YPS na Wanawake Amani na Usalama, WPS,utakamilika kesho, Agosti 12, 2026, katika Ikulu ya Kiriri mjini Bujumbura, nchini Burundi.

Mkutano huo, unaoandaliwa na Umoja wa Afrika, AU kwa ushirikiano na Serikali ya Burundi chini ya uenyekiti wa Rais Évariste Ndayishimiye, umejikita katika usimamizi wa rasilimali za maji, uongozi shirikishi na ujenzi wa amani endelevu.

Ukiendeshwa chini ya kaulimbiu “Maji, Amani na Uongozi Shirikishi barani Afrika” mkutano huo unachunguza uhusiano kati ya uhaba wa maji, migogoro na amani, huku ukisisitiza nafasi muhimu ya vijana na wanawake katika kuzuia migogoro, kudhibiti misukosuko na kusimamia rasilimali.

Mkutano huo umewaleta pamoja watunga sera barani Afrika, wawakilishi wa Baraza la Amani na Usalama la AU, wajenzi wa amani wanawake, viongozi vijana, mashirika ya kikanda, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, wasomi na washirika wa maendeleo.

Washiriki wa mkutano huo ulioanza jana Agosti 10, 2026, wanalenga kuimarisha utekelezaji wa ajenda za Vijana, Amani na Usalama, YPS na Wanawake, Amani na Usalama, WPS, kukuza ushirikiano wa vizazi mbalimbali na kuandaa mapendekezo ya vitendo ya kuwaunganisha vijana na wanawake katika mifumo rasmi ya amani na usalama.

Mkutano huo utahitimishwa kwa kupitishwa kwa taarifa ya bara yenye mapendekezo na ahadi muhimu. Siku yake ya mwisho pia itaambatana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana 2026.

Share This Article