Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI imetangaza kukamatwa kwa washukiwa wengine watatu kuhusiana na mauaji ya Dkt. Victoria Nthunya Mutiso, katika operesheni iliyofanyika Nairobi na Kampala.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X, DCI ilifafanua kwamba washukiwa wawili, Konstebo wa Polisi Bett Kiplangat Collins na raia Pius Muiru Mbugua, walikamatwa Kampala kwa ushirikiano wa Polisi wa Uganda.
Wawili hao wanadaiwa kukimbilia Uganda baada ya mauaji hayo na kwa sasa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Jinja Road, wakisubiri kurejeshwa nchini Kenya chini ya ulinzi.
Mtuhumiwa wa tatu, Samuel Karanja Gathoni, maarufu kama “Lawyer”, alikamatwa katika eneo la Langata Multi-Media jijini Nairobi alipokuwa akielekea Ongata Rongai.
Kwa mujibu wa DCI, Konstebo Bett alipatiwa jukumu la kufanya ufuatiliaji na alikuwa dereva msaidizi wa Daniel Mwangi Njoroge, ambaye wachunguzi wanamtaja kuwa mmoja wa waandaaji wakuu wa operesheni hiyo ya mauaji.
Inadaiwa Njoroge alikuwa akiendesha gari aina ya Land Cruiser Prado, lenye nambari ya usajili KDH 600A, lililotumika kuizuia teksi iliyokuwa imembeba Mutiso, muda mfupi kabla ya kupigwa risasi na kuuawa katika eneo la Upper Hill Julai 29, 2026.
Wachunguzi pia wanadai kuwa Mbugua alikuwa msimamizi wa malipo, akiratibu fedha na mahitaji ya usafirishaji na shughuli nyingine za timu iliyodaiwa kuhusika katika mauaji hayo.
DCI imesema washukiwa hao watatu watafanyiwa taratibu zinazohitajika na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.