Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imepata agizo la mahakama kumzuilia mshukiwa wa uchochezi wa ukabila kwa siku kumi, ili kutoa fursa uchunguzi kufanywa kuhusiana na madai hayo.
Mahakama ya Hakimu Mkuu wa Kahawa iliagiza Bare Sahara Ahmed anayetuhumiwa kutoa matamshi ya chuki na uchochezi wa kikabila, azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani.
Aidha mahakama hiyo iliagiza kufanywa kwa uchunguzi wa kisayansi kwa vifaa vyake vya kidijitali ikiwa ni pamoja na deta ya mawasiliano ya simu na ile ya kifedha kupiga jeki uchunguzi huo.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema hatua hiyo inaonyesha lengo la serikali la kudumisha uzingatiaji wa sheria na kushughulikia makosa yanayotishia umoja wa kitaifa na utangamano wa amani.
“Tunatoa wito kwa wananchi kuwajibika katika mawasiliano yao na kuepuka kujihusisha na maswala yanayochochea migawanyiko au chuki,” ilisema DCI.