Ragga Dee azungumzia machozi ya kinafiki mazishini

Amekosoa hulka ya watu kuomboleza kwa huzuni kubwa mtu akifariki, ilhali alipokuwa hai walimpuuza, kumdharau au hata kufurahia matatizo yake

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki mkongwe nchini Uganda ambaye pia ni mwanasiasa Daniel Kazibwe, maarufu kama Ragga Dee amezungumzia kile anachokitaja kuwa machozi ya kinafiki kwenye hafla za mazishi.

Msanii huyo amekosoa hulka ya watu kugeuka ghafla kuwa waombolezaji wenye huzuni kubwa baada ya mtu kufariki, ilhali alipokuwa hai walimpuuza, kumdharau au hata kufurahia matatizo yake.

Akizungumza kwenye kipindi cha mitandaoni, mwanamuziki huyo mwenye msimamo mkali alihoji ni kwa nini watu husubiri mtu afe ndipo waonyeshe hisia ambazo hawakuwahi kuzionesha akiwa hai.

Ragga Dee alielekeza lawama zake kwenye tasnia ya muziki, akidai kwamba baadhi ya wasanii hufurahia kwa siri mwanamuziki mwenzao anapokumbwa na matatizo, lakini mtu huyo akifariki hujitokeza na kuonekana kama wamevunjika moyo.

Aliwataka watu kuacha kujifanya na badala yake wawe waaminifu katika mahusiano yao wakati bado wana nafasi.

Ragga Dee, aliyewahi kuwania wadhifa wa Meya wa jiji la Kampala anasema kama humpendi mtu, hutaki kufanya naye kazi, unamdharau au unaamini amekukosea, mwambie akiwa hai. Usisubiri jeneza lake ndipo ghafla uanze kuonyesha mapenzi makubwa.

Alimtaja mtengenezaji filamu mkongwe Alex Mukulu kama mtu aliyemfundisha umuhimu wa kusema ukweli bila kuficha.

Ragga Dee hata alitania kuwa kama wafu wangeweza kujibu, baadhi yao huenda wangewashika tai wanaoweka maua kwenye jeneza na kuwauliza yalipokuwa mapenzi hayo wakiwa hai.

Share This Article