Polisi wafanya kampeni ya uhamasisho wa usalama barabarani

Martin Mwanje
1 Min Read

Idara ya Trafiki imefanya kampeni ya kitaifa ya uhamasisho wa usalama barabarani wakati ambapo kumekuwa visa vilivyoongezeka vya ajali zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini. 

Kampeni hiyo ilifanywa jana Jumatatu na maafisa wa trafiki kutoka kaunti za Makueni, Machakos, Marsabit, Nyeri, Murang’a, Kirinyaga, Kiambu, Kwale na Nyandarua.

Wote hao walishiriki mazungumzo na watumiaji wa barabara, ikiwa ni pamoja na wanabodaboda na waenda kwa miguu, katika hatua iliyolenga kuwasihi kutii sheria za barabarani na kuwajibika wanaposafiri.

Masuala yaliyotiliwa maanani wakati wa kampeni hiyo ni pamoja na tabia ya jumla ya watumiaji barabara, kuheshimu sheria za trafiki na kuepuka kuendesha vyombo vyao vya usafiri kwa kasi na kubeba watu kupita kiasi.

Huduma ya Taifa ya Polisi inatoa wito kwa madereva kuwa waangalifu na kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri wakati wakitii sheria za barabarani hasa msimu wa mvua za El Nino unapokaribia.

Share This Article