Maafisa wa Polisi wamewakamata washukiwa wanne kwa madai ya kuhusika na ulanguzi wa mihadarati katika kaunti ya Busia na Bungoma.
Katika kaunti ya Busia, maafisa hao kutoka idara ya kitaifa ya uchunguzi dhidi ya ulanguzi wa mihadarati (NANIB), walisimamisha lori aina ya Fuso lililokuwa likisafirisha nafaka kuelekea Nairobi lenye nambari za usajili KDU 981Y, kwenye Barabara Kuu ya Busia–Kisumu.
Baada ya kulipekua lori hilo, maafisa hao walipata mifuko 14 ndani ya magunia mawili iliyokuwa na bangi. Magunia hayo yalikuwa yamefichwa chini ya mihogo iliyokaushwa ili kuzuia kutambuliwa upesi.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imesema bangi hiyo yenye uzani wa kilo 59.15, ni ya thamani ya shilingi 1,774,500.
“Washukiwa wawili Evans Josiah Mugambi na Moses Murambula Odwera, walikamatwa na wanazuiliwa kwenye korokro za polisi,” ilisema DCI.
Katika kaunti Jirani ya Bungoma, maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria katika barabara ya Siritanyi–Mateka, ambapo walisimamisha gari aina ya Toyota Probox, lenye nambari za usajili KCK 089M.
Na baada ya kulipekua walipata mifuko 5 iliyokuwa na bangi ya uzani wa kilo 7. Washukiwa wawili Boaz Kwamba na Peter Ndungu, walikamatwa na wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi.
Washukiwa hao wanne wanasubiri kufikishwa mahakamani, huku mihadarati hiyo ikizuiliwa na itatumika kama Ushahidi kwenye kesi dhidi ya washukiwa hao.