Masomo katika vyuo vikuu vya umma yalilemazwa leo Ijumaa baada ya wahadhiri na wafanyakazi zaidi ya 30,000 wa vyuo hivyo kote nchini kususia kazi.
Wote hao wanashinikiza kutekelezwa kwa Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2025-2029 wanaosema utawanyea mvua ya pesa nyingi ikiwa utatekelezwa.
Wahadhiri na wafanyakazi wanaogoma ni wanachama wa vyama vya UASU, KUSU na KUDHEHIA.
Walitoa ilani ya kuanza mgomo huo Oktoba 2 baada ya kukwama kwa mazungumzo kati ya vyama hivyo na Kongamano la Mabaraza ya Vyuo Vikuu (IPUCCF).
Katika kutoa ilani hiyo, wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma nchini walitaja kucheleweshwa kwa mazungumzo hayo, kusajiliwa kwake na kutekelezwa kwa CBA ya mwaka 2025-2029.
Katika Chuo Kikuu cha Murang’a, madarasa yalisalia mahame wakati wahadhiri wakijiunga na wenzao nchini kote kushinikiza kuangaziwa kwa maslahi yao.
Akiwahutubia wanahabari, Katibu wa UASU tawi la Murang’a Dkt. Stephen Njenga alisema kamwe hawatarejea kazini hadi malalamishi yao yatafutiwe ufumbuzi.
Alielezea kuwa CBA ya mwaka 2025-2029 , ambayo mazungumzo yake yalitarajiwa kuwa tayari yamekamilika baada ya makubaliano ya kurejea kazini kufikiwa na IPUCCF mwezi Novemba mwaka jana, bado haijashughulikiwa.
Dkt. Njenga aliituhumu Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC kwa kuchelewesha mchakato huo na kutoa wito wa kutekelezwa kwake mara moja.
Huku kukiwa na mivutano kati ya IPUCCF na vyama vya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma, haijulikani ni lini mgomo unaoendelea utamalizika, huku wanafunzi wengi waliotazamia kumaliza masomo yao kwa wakati uliopangwa, sasa wakianza kuhangaika.