Mudavadi ahimiza Wamaasai kudai maendeleo mwaka 2027

Aliwahimiza pia kujiandikisha kama wapiga kura, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuwapima viongozi wa kisiasa kwa rekodi yao ya maendeleo.

Marion Bosire
1 Min Read

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, amewataka watu wa jamii ya Maa katika Kaunti ya Narok kutumia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 kuwachagua viongozi wanaoweza kuleta maendeleo yanayoonekana.

Mudavadi alisema hayo huko Motonyi, Narok, alipoungana na familia ya aliyekuwa Waziri marehemu William ole Ntimama, wanajamii wa Maa na viongozi wengine kuadhimisha miaka 10 tangu kifo cha Ntimama na kuzindua wasifu wake.

Alielezea urithi wa Ntimama kuwa uliojikita katika heshima, haki za ardhi, kutambuliwa, heshima ya kisiasa na uwezeshaji wa jamii.

Nchi inapojitayarisha kwa uchaguzi wa 2027, Mudavadi aliwahimiza Wamaasai kujiandikisha kama wapiga kura, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuwapima viongozi wa kisiasa kwa rekodi yao ya maendeleo badala ya ahadi za kampeni.

Alisema utajiri mkubwa wa Narok, ukiwemo utalii, ufugaji, kilimo na ardhi, unapaswa kuleta ajira zaidi, biashara na fursa, hasa kwa vijana.

Mudavadi pia alitaka wenyeji washirikishwe zaidi katika sekta ya utalii ili wakazi wa Narok wanufaike kikamilifu na utajiri wa utalii wa kaunti hiyo.

Aliwahimiza Wamaasai kutetea maslahi yao bila kuchochea uhasama dhidi ya jamii nyingine na kudai mgao wao wa rasilimali za kitaifa huku wakiheshimu haki za Wakenya wengine.

Alisema mtazamo huo unaakisi urithi wa Ntimama wa heshima, ushiriki, umoja na uwezeshaji.

Share This Article