Raia 6 wa Iran wakabiliwa na kesi ya Meth ya Bilioni 8.2

Wanadaiwa kusafirisha kilogramu 1,036.044 za dawa ya methamphetamine yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 8.2.

Marion Bosire
2 Min Read

Raia sita wa Iran wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha zaidi ya tani moja ya dawa ya methamphetamine wamepatikana na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Shanzu.

Hakimu Mkuu wa Shanzu, Anthony Mwicigi, aliamua kuwa upande wa mashtaka umeweka ushahidi wa awali wa kutosha dhidi ya washtakiwa hao sita, na hivyo kuwawezesha kuanza kujitetea chini ya Kifungu cha 211 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Washtakiwa hao ni Jaseem Darzadeh Nia, Nadeem Jadgal, Hassan Baloch, Raheem Baksh, Imran Baloch na Imtiyaz Daryay.

Wanadaiwa kusafirisha kilogramu 1,036.044 za methamphetamine zenye thamani ya takriban shilingi bilioni 8.2, kinyume na Kifungu cha 4(a)(ii) cha Sheria ya Dawa za Kulevya na Dawa za Kisaikolojia.

Mahakama iliafikia uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kuwaita mashahidi 12 na kufunga ushahidi wake.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa washtakiwa hao, pamoja na watu wengine, walisafirisha mzigo huo kwa kutumia meli ya Mashaallah, ambayo inadaiwa kutosajiliwa na haikuwa na uraia wa nchi yoyote.

Meli hiyo ilikamatwa katika bahari kuu ikiwa imebeba dawa hizo za kulevya kati ya Oktoba 17 na 20, 2025, katika maji ya kimataifa.

Hakimu Mwicigi alieleza kuwa kesi hiyo ni ya kipekee kutokana na ukubwa wake na ukweli kwamba ushahidi uliowasilishwa ulitokana na bahari kuu.

Upande wa mashtaka unaongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Joseph Kimanthi.

Share This Article