Wauguzi katika Hopitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH), wamesitisha mgomo baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kurejea kazini kati ya chama chao na usimamizi wa hospitali hiyo.
Tangazo hilo lilitolewa Jumanne jioni na Waziri wa Afya Adan Duale, aliyesema makubaliano hayo yaliafikiwa baada ya majadiliano ya kina.
Makubaliano hayo yanajumuisha sehemu muhimu kama vile, kuimarishwa kwa bima ya afya, wauguzi kupandishwa vyeo, mikakati ya kukabiliana na changamoto kazini na kuwaajiri kwa masharti ya kudumu wauguzi walio kwenye kandarasi.
“Kwa niaba ya Wizara ya Afya, nayashukuru makundi yaliyoongoza majadiliano hayo kwa kuonyesha nia njema, utaalam na kujitolea kutatua maswala yaliyokuwepo,” alisema Duale.
Aidha, waziri huyo alihakikisha kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote kutekeleza kikamilifu maazimio yaliyokubaliwa katika muda uliowekwa.
Huduma za kawaida zimerejea katika hospitali hiyo, baada ya wauguzi hao kurejea kazini.