Erling Halaand alipachika mabao mawili ya kipindi cha pili na kuisaidia Norway kuwatema nje mabingwa mara tano Brazil 2-1 na hivyo kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza Jumapili usiku.
Brazil, walioonekana kunyong’onyea kuanzia kipenga cha mwanzo uwanjani New Jersey, watajilaumu baada ya Bruno Guimares kushuhudia penalti yake ya kipindi cha kwanza ikipanguliwa na kipa wa Norway, Orjan Nyland.
Kipindi cha pili, Samba Boys ya Brazil walijaribu kila mbinu kuvunja ngome ya Norway iliyokaa tisti na kukataa abadan kutoa fursa ya kufungwa.
Hata hivyo, Halaand alipata fursa ya mwaka alipounganisha kwa kichwa pasi ya Andreas Schjelderup dakika ya 79 na kuwaweka uongozini na kuongeza la pili kwa kufyatua tobwe la pembeni kulia kunako dakika ya 90.
Brazil walipata goli la kufuta machozi dakika ya 10 ya mazidadi kupitia penalti yake Neymar Junior, lakini hawakuwa na muda wa kusawazisha.
Norway watachuana na Uingereza iliyoishinda Mexico kwa magoli 3-2 katika robo fainali.
Upande mwingine, Brazil wataendelea na subira ya kombe la sita la dunia tangu watwae la tano mwaka 2002.