Timu ya taifa ya Raga ya Kenya kwa wachezaji saba upande wa wanaume almaarufu Shujaa, itaanza harakati za mwisho kurejea kwa mashindano ya dunia leo katika mkondo wa Bordeaux nchini Ufaransa.
Kenya inayonolewa makali na Kevin Wambua, itafungua mkondo huo kundini A dhidi ya Fiji kuanzia saa tisa na dakika 44 alasiri, kabla ya kukabiliana na Afrika Kusini saa tatu na dakika 46 usiku.
Shujaa watamaliza ratiba ya kundi lao dhidi ya Uingereza saa tano na dakika 44 siku ya Jumamosi.
Kenya ambayo ni ya nane kwenye jedwali, inahitaji kumaliza katika nafasi ya nane katika mkondo huo, ili kufuzu kurejea kwa mashindano ya Msururu wa Dunia msimu ujao.