Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wamemkamata Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Miji na Mipango wa serikali ya kaunti ya Nairobi, akiwa na kitita cha shilingi milioni 65.3 nyumbani kwake eneo la Syokimau, kaunti ya Machakos.
Kulingana na EACC, operesheni hiyo ilitekelezwa nyumbani kwa Patrick Analo Akivaga kama sehemu inayoendelea ya uchunguzi dhidi ya uhalifi wa kiuchumi katika kaunti hiyo.
Kupitia kwa taarifa iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Abdi Mohamud, EACC ilisema inachunguza madai ya mkinzano wa maslahi, utumizi mbaya wa mamlaka, ulaji rushwa na umiliki wa mali unaotiliwa shaka dhidi ya afisa huyo.
“Inadaiwa kuwa Akivaga hupokea mamilioni ya fedha kupitia pesa taslimu na kupitia mfumo wa M-pesa,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, taarifa hiyo iliongeza kuwa afisa huyo anamiliki mali ambayo haiambatani na mapato yake halali.
Kwenye msako huo, tume hiyo ilipata shilingi milioni 53 na dola 113,000 za Kimarekani ambazo ni sawa na shilingi milioni 14 nyumbani kwake Syokimau.
“Vitu vingine vilivyopatikana kwenye operesheni hiyo ni pamoja na hatimiliki za ardhi, hati za kumiliki magari, vipakatalishi, makubaliano ya kuuza magari na mashamba, simu za mkononi, na vifaa vingine vya kielektroniki miongoni mwa vingine,” iliongeza taarifa hiyo.
EACC imesema inaendelea na uchunguzi kubaini hatua ambayo itachukuliwa punde uchunguzi utakapokamilika.