Watu sita wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gari la kuwabeba abiria kushambuliwa katika eneo la Ber Cawayon, Harer i Hosle, kaunti ndogo ya Arabia, kaunti ya Mandera.
Gari hilo ambalo lilikuwa likisafiri kuelekea Arabia mjini, lilishambuliwa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki Jumamosi mchana, kisa ambacho kimewashangaza wengi.
Miili ya waliofariki ilipelekwa katika hifadhi ya maiti katika hopsitali ya kaunti ndogo ya Arabia, huku waliojeruhiwa pia wakiwasilishwa kwenye hospitali hiyo kwa matibabu ya dharura.
Kundi la maafisa kutoka asasi mbali mbali za kiusalama, lilipelekwa haraka katika eneo hilo kuwatafuta wavamizi hao na kubaini chanzo cha shambulizi hilo.
Majina ya waathiriwa wa shambulizi hilo bado hayajatolewa na maafisa wa utawala, huku uchunguzi wa kisa hicho ukianza mara moja.