Rais William Ruto amekamilisha ziara ya siku tatu kaskazini mwa Kenya huku akielezea kujitlea kwa serikali kumaliza kutengwa kwa eneo hilo kupitia uwekezaji endelevu katika miradi ya maendeleo.
“Pamoja tutaendelea kufungua uwezo wa Kaskazini mwa Kenya na kuhakikisha hakuna eneo ambalo linaachwa nyuma katika safari ya kuleta mageuzi hapa nchini,” alisema Rais Ruto.
Kwenye ziara yake siku ya mwisho, kiongozi wa taifa alikagua ujenzi wa barabara ya kilomita 257 kutoka Lamu-Ijara-Garissa, ikiwaa ni sehemu ya kilomita 453 ya mradi wa maendeleo wa LAPSSET.
Rais alisema mradi huo utakaogharimu shilingi bilioni 17.9, unatarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao na unatarajiwa kuleta njia mbadala ya uchukuzi, kupiga jeki utangamano wa eneo hilo, kuimarisha usalama na kutoa mfumo wa usafiri kwa bandari ya Lamu.
Awali kiongozi wa nchi alidokeza kuwa serikali inawekeza shilingi bilioni 4.1 katika kaunti ya Wajir ili kuunganisha nyumba 26,000 kwa stima, huku nyumba 18,600 zikiunganishwa kwa stima katika kaunti ya Mandera kwa kitita cha shilingi bilioni 2.5, na nyumba 8,300 zikiunganishwa na stima katika kaunti ya Garissa kwa shilingi bilioni 1.6.
Baadaye aliwahutubia wakazi wa Lagdera, akiwafahamisha kuhusu miradi ya maendeleo katika eneo la Garissa.