Tume ya Maadili na vita dhidi ya Ufisadi hapa nchini (EACC), imetwaa ardhi ya umma katika kaunti ya Kisumu yenye thamani ya shilingi milioni 25, iliyouzwa kinyume cha sheria.
Ardhi hiyo ya hekari 0.1116 inayomilikiwa na Shirika la Reli nchini, ilitwaliwa baada ya kuamuliwa kwa kesi na Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Kisumu.
Katika hukumu iliyotolewa Machi 20, 2025, Jaji Samson Okong’o, aliagiza kufutiliwa mbali kwa hatimiliki ya ardhi nambari 7/559, ambayo ilitolewa kinyume cha sheria kwa Fred Ogonji.
Mahakama hiyo ilithibitisha kuwa ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya ardhi iliyotengewa Shirika la Reli nchini.
Uchunguzi wa EACC umebainisha kuwa ardhi hiyo awali ilimilikiwa na iliyokuwa Shirika la Reli la Afrika Mashariki chini ya ilani ya kisheria nambari 440 ya mwaka 1963.
Mnamo mwaka 1986, ilihamishwa hadi kwa Shirika la reli la Kenya kupitia ilani ya kisheria nambari 24 ya mwaka 1986.