Bitok: Shule hazitafungwa mapema kwa likizo ya katikati ya muhula

Prof. Bitok amesema Wizara ya Elimu imeingilia kati kurejesha hali ya utulivu, kulinda elimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanasalia shuleni.

Tom Mathinji
2 Min Read
Katibu katika Wizara ya Elimu Julius Bitok akiwa katika shule ya upili ya Kenya High.

Katibu katika Idara ya Elimu ya Msingi Prof. Julius Bitok amesema kuwa shule hazitafungwa mapema kwa mapumziko ya katikati ya muhula. 

Amesema shule nyingi zinaendelea na ratiba yao ya kawaida licha ya taharuki kushuhudiwa katika baadhi ya shule nchini.

Akizungumza leo Alhamisi katika shule ya upili ya Kenya High wakati wa hafla ya kuwatuza wanafunzi, Prof. Bitok  alisema wizara hiyo imeingilia kati kwa ushirikiano na wadau wengine kurejesha hali ya utulivu, kulinda elimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanasalia shuleni.

“Lengo letu ni wazi, kulinda haki ya kila mtoto kuhakikisha anapata elimu, kuimarisha uthabiti katika taasisi zetu na kukabiliana na changamoto ibuka na uwajibijaki,” alisema Katibu huyo.

Alidokeza kuwa bidii ya wanafunzi hao, inachochea serikali kuhakikisha mazingira salama na bora ya elimu kote nchini.

Matamshi yake yanajiri huku taharuki ikishuhudiwa katika baadhi ya shule kote nchini. Katika shule ya wasichana ya Utumishi Girls Academy, kaunti ya Nakuru, wanafunzi kadhaa wanadaiwa kuteketeza bweni na kusababisha vifo vya wanafunzi 16 na zaidi ya 70 kujeruhiwa.

Shule ya upili ya wavulana ya Alliance nayo imefungwa kwa muda kufuatia tukio la moto kwenye hifadhi ya magodoro madogo kwenye mojawapo ya mabweni ya zamani shuleni humo.

Kwa upande mwingine, wanafunzi wa shule za upili za wasichana za Nakuru na Njoro wameagizwa kwenda nyumbani katika hali tatanishi.

Share This Article