Usimamizi wa shule ya upili ya wavulana ya Alliance High umeazimia kuwataka wanafunzi wa shule hiyo kwenda nyumbani kufuatia kisa cha moto kilichotokea shuleni hapo mapema leo asubuhi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo anasema moto huo ulitokea kwenye eneo dogo lenye magodoro katika moja ya mabweni ya zamani.
Ameongeza kuwa moto huo, ambao chanzo chake bado hakijulikani, ulidhibitiwa haraka na kwamba hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa.
Kufuatia kisa hicho, Bodi ya Usimamizi na Utawala wa Shule hiyo uliitisha mkutano wa wazazi leo Alhamisi, majira ya saa nne asubuhi, ili kuwaarifu kilichotokea na hatua zilizochukuliwa.
“Kufuatia mkutano huo, wazazi wameombwa kwenda na wanao nyumbani na kukaa nao wikendi hii. Hatua hii inadhamiria kutoa fursa ya wanafunzi kuwa na wazazi wao wakati shule ikipitia upya taratibu za ndani na maandalizi kuhakikisha shughuli zinaendelea kama kawaida na kuwepo kwa mandhari mazuri ya kusomea,” alisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye hakujitambulisha kwenye taarifa.
Aidha, Mwalimu Mkuu huyo amewataka wazazi kutohofu, kwani shule hiyo inatoa kipaumbele kwa usalama wa wanafunzi.
Kisa hicho kinajiri siku chache baada ya mkasa wa moto kusababisha vifo vya wanafunzi 16 katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil katika kaunti ya Nakuru.
Wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa kwenye mkasa huo.
Wanafunzi 9 wamefikishwa mahakamani na wanazuiliwa kwa siku 21 ili kupisha uchunguzi kufuatia madai ya kusababisha mkasa huo.