Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha azimio la kumzuia Rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 215 dhidi ya 208, baada ya wabunge wanne wa chama anachotoka Trump cha Republican kuungana na wale wa Democrat katika hatua ya nadra ya kupinga hadharani vita hivyo.
Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilianza mwishoni mwa mwezi Februari.
Hata hivyo, azimio hilo bado linahitaji kupitishwa na Bunge la Seneti, linalodhibitiwa na Republican. Hata likipitishwa huko, Trump anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu kuzuia azimio hilo kuwa sheria, jambo ambalo linahitaji theluthi mbili ya kura katika mabunge yote mawili ili kubatilishwa.
Wabunge wa Republican Thomas Massie, Brian Fitzpatrick, Tom Barrett na Warren Davidson waliungana na wabunge wa Democrat kuunga mkono azimio hilo. Barrett alisema ni jukumu la Bunge pekee kutangaza vita na kwamba alipiga kura kulingana na dhamiri yake, bila kujali shinikizo lolote la kisiasa.
Mbunge Gregory Meeks wa Democrat alieleza kura hiyo kama pigo kubwa kwa Trump, akisema vita dhidi ya Iran vimekuwa vya gharama kubwa, havijafanikisha malengo yake yaliyotangazwa na vimeongeza ugumu wa kupata suluhisho la kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Pia alisema wabunge wengi wa Republican wanaanza kusikiliza wapiga kura wao ambao hawataki vita vingine vya muda mrefu Mashariki ya Kati.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana katika siku za karibuni.
Akizungumza kutoka Ikulu ya Marekani, Trump alisema mazungumzo ya kumaliza vita yanaendelea vizuri na yanaweza kukamilika mwishoni mwa wiki hii, akiongeza kuwa pande zote ziko karibu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo.
Taarifa ya BBC