Kenya na Urusi zinajizatiti kuimarisha ushirikiano baina yao katika sekta za elimu, biashara, nishati na utamaduni, huku uhusiano wa nchi hizo mbili ukiendelea kuimarika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya Urusi Jijini Nairobi, balozi wa Urusi nchini Kenya Vsevolod Tkachenko, alisema nchi hizo mbili zimepiga hatua ya kumezewa mate katika siasa, uchumi na ushirikiano wa utamaduni kwa muda mrefu.
Balozi huyo alitaja Kenya kuwa mojawepo wa chumi bora zaidi barani Afrika na mshirika muhimu wa Urusi katika kanda ya Afrika Mashariki.
“Ninafahari kusema kuwa tumekuwa na uhusiano mwema wa kirafiki kati ya Russia na Kenya. Kwa muda mrefu, ushirikiano huo umekuwa ukipiga hatua,” alisema Tkachenko.
Aidha, alitaja ziara ya Jijini Moscow ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi, kuwa hatua muhimu ya kufungua fursa mpya za mashauriano ya kiuchumi na ushirikiano thabiti.
Kulingana na balozi huyo, ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili ulifikia dola milioni 600 mwaka 2025, ukipigwa jeki na bidhaa zinazoingizwa hapa nchini kutoka Russia za ngano na mbolea, huku Kenya ikiuza nchini Russia maua, Majani Chai na Kahawa.
“Kuna uwezekano wa kupanua ushirikiano katika sekta hizi, ambao hautaleta tu manufaa kwa pande zote lakini utahakikisha utoshelevu wa chakula katika kanda ya Afrika Mashariki,” alisema balozi huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa maswala ya kidiplomasia katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Josphat Maikara, aliyemwakilisha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi katika maadhimisho hayo, alisema Kenya imejitolea vilivyo kupanua ushirikiano wake na Russia katika sekta mbali mbali.
“Ushirikiano wetu unahusisha sekta muhimu kama vile biashara, uwekezaji, ulinzi, elimu na utalii,” alisema Maikara.
Maadhimisho hayo yaliwleta pamoja wanadiplomasia, maafisa wa serikali, viongozi wa kibiashara, wasomi, wanahabari raia wa Urusi na marafiki wa Urusi.