Rais William Ruto amesema Afrika haina uhaba wa mtaji wa kulibadilisha bara hilo kimaendeleo.
Badala yake, Ruto ameelezea kuwa tatizo la Afrika ni sheria zinazoamua ni wapi “mtaji huo unapaswa kwenda”.
Ameelezea kuwa utafiti uliofanywa na shirika la African Finance Corporation (AFC) umethibitisha kuwa Afrika ina rasilimali zinazohitajika za kuweka msingi wa kustawi kiuchumi.
Rais Ruto aliyasema hayo wakati wa ‘mkutano wa Ngazi ya Juu wa Africa We Build’ ulioandaliwa na AFC pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.

Alielezea kuwa kile Afrika inakosa ni uwekezaji wenye mpangilio na mpango wa kushirikishana hatari badala ya mtaji halisi.
“Mtaji wa Afrika usiotoka kwenye benki ndani ya bara hilo umezidi dola trilioni 2, na mali zetu za pensheni na bima zimezidi trilioni 1 kwa mara ya kwanza katika historia yetu,” alisema Rais Ruto.
Alisema fedha zote kutoka nje ya bara hilo kati ya mwaka 2014 na 2024, za misaada na kibiashara kwa pamoja, zilikuwa jumla ya dola trilioni 1.7.
“Akiba zetu sasa ni kubwa kuliko pesa za watu wengine. Ilhali pesa za watu wengine zinapungua kwa sababu Usaidizi Rasmi wa Maendeleo umekuwa ukipungua kila mwaka tangu mwaka 2020,” aliongeza Ruto.
Wakati wa mkutano huo, Rais alilalama kuwa sheria za kifedha zinaelekeza akiba za pensheni barani Afrika kuelekea dhamana za serikali badala ya maendeleo ya miundombinu hata wakati sheria zinaruhusu uwekezaji mkubwa katika miradi.