Owino: Serikali imeimarisha juhudi za kukabiliana na El Nino

Shirika la Utabiri wa hali ya Hewa limetangaza kuwa mvua za El Nino zitaanza mwezi Oktoba na kukamilika mwezi Disemba, kukiwa na uwezekano wa kuendelea hadi mapema mwaka ujao.

Tom Mathinji
2 Min Read
Charles Owino - Msemaji wa serikali.

Serikali imetangaza kuwa imeimarisha juhudi za kukabiliana na mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.

Kwenye mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi, Msemaji wa serikali Charles Owino alisema mipango ya pamoja inayoshirikisha wizara na idara husika za serikali, serikali za kaunti, mashirika ya kibinadamu na washirika wa kimaendeleo, imewekwa kuhakikisha athari zitakazosababishwa na mvua hizo zinakabiliwa vilivyo.

Aidha, alitoa wito kwa Wakenya kuchukua tahadhari za mapema ili kulinda maisha na kuzuia uharibifu wa mali.

“Serikali inatoa wito kwa Wakenya kufanya maandalizi ya mvua za El Nino kuwa jukumu la pamoja,” alisema Owino.

Kulingana na Owino, serikali inaendelea kutambua maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko, huku ikijiandaa kukabiliana na majanga, ikiwa ni pamoja na kutoa habari za mapema kwa jamii husika.

“Wananchi wanashauriwa kutegemea habari zinazotolewa kupitia mifumo ya serikali na wajiepushe kueneza habari potovu,” alidokeza msemaji huyo wa serikali.

Wakati huo huo wananchi wameshauriwa kuepuka kuvuka mito iliyofurika, kutembea au kuendesha gari kwenye maji yanayotiririka kwa kasi, kuweka vyema stakabadhi muhimu na kutilia maanani maagizo ya uokoaji kutoka kwa maafisa wa serikali.

Shirika la Utabiri wa hali ya Hewa limetangaza kuwa mvua za El Nino zitaanza mwezi Oktoba na kukamilika mwezi Disemba, kukiwa na uwezekano wa kuendelea hadi mapema mwaka ujao.

Share This Article