Wakazi Machakos walipa bunge na Gavana makataa ya maelewano

Mashirika ya kijamii yametoa makataa ya siku 10 kwa bunge na serikali ya kaunti kuelewana kuhusu bajeti au yaelekee kortini kulazimisha maelewano

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi wa kaunti ya Machakos wanaripotiwa kuendelea kukusanyika nje ya bunge la kaunti ya Machakos ambapo hali ya taharuki inaendelea kutanda wakishinikiza maelewano kati ya Gavana na bunge.

Usimamizi wa bunge hilo la kaunti ya Machakos nao umetishia kuzuia waandishi wa habari kuingia bungeni humo baada ya Gavana Wavinya Ndeti kufika huko Jumatatu akiwa ameandamana na wanahabari kulalamikia bajeti iliyopitishwa.

Jana spika wa bunge hilo Ann kiusya alitangaza kuwa bunge hilo linawaza kuwazuia waandishi wa habari kutokana na tukio hilo la Jumatatu ambapo Gavana anadaiwa kulazimisha kupokelewa kwa barua za kukataa bajeti iliyopitishwa nusu.

Kwa sasa makundi ya watu yanaendelea kukusanyika nje ya bunge hilo mashirika ya kijamii yakitoa makataa ya siku kumi kwa bunge hilo na serikali ya kaunti kuelewana kuhusu bajeti au waelekee kortini kulazimisha maelewano.

Gavana Ndeti alikataa kutia saini bajeti hiyo ya shilingi Bilioni 17.8 akilaumu wabunge wa bunge hilo la kaunti kwa kubadili mipango ya matumizi ya fedha za kaunti kinyume cha sheria.

Wawakilishi wadi hao wanadaiwa pia kuelekeza shilingi milioni 854 zilizokuwa zimetengewa huduma muhimu kwa matumizi tofauti.

Fedha zilizokuwa zimetengewa hazina ya Wikwatyo na mipango ya kuwezesha wanawake na vijana zilipunguzwa kutoka shilingi milioni 274 hadi milioni 74, pesa za ufadhili wa elimu zikapunguzwa kwa milioni 30 huku miradi ya barabara pia ikipunguziwa fedha.

Ndeti analaumu bunge la kaunti pia kwa kujiongezea fedha katika hazina yake ya maendeleo kwa shilingi milioni 130 huku akirejesha mswada huo bungeni kwa utathmini na marekebisho.

Share This Article