Washukiwa watatu zaidi wamefikishwa katika mahakama ya Milimani kuhusiana na mauaji ya Dkt. Victoria Mutiso wakati uchunguzi wa mauaji hayo ukipamba moto.
Watatu hao ni Pius Mbugua, Samwel Karanja almaarufu Wakili na Polisi Konstebo Collins Bet.
Mbugua na Bet ni maafisa wa polisi wanaohudumu katika kituo cha polisi cha Thogoto.
Wawili hao walikamatwa mjini Kampala nchini Uganda Agosti 29 huku Karanja akikamatwa katika eneo la Multimedia, eneo bunge la Langata.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inataka watatu hao kuzuiliwa wakati uchunguzi wa kubaini jinsi Dkt. Mutiso alivyokumbana na mauti ukishika kasi.
Mwanasiasa Rose Mbithe Mulwa almaarufu Rose Mbithe Ndetei na wanawe Chris Mulwa na Agnes Mulwa tayari wanazuiliwa kuhusiana na mauaji hayo.
Dkt. Mutiso aliuawa na watu wasiojulikana katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi Julai 29 mwaka huu.
Uchunguzi wa DCI uliashiria kuwa Mbithe na wanawe walikula njama na maafisa wa polisi kumuua Dkt. Mutiso mwishoni mwa mwezi Julai.
Uchunguzi umebaini kuwa kiini cha mauaji hayo ni mzozo wa ardhi iliyopo katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.
DCI inaamini kuwa ni mzozo huo ambao yamkini ulisababisha kifo cha wakili Kyalo Mbobu mwezi Septemba mwaka jana.
Taarifa hii imechangiwa na mwanahabari wetu John Kahiro.