Rais William Ruto amepuuzilia mbali wale wanaotilia shaka tangazo lake kwamba masomo ya wanafunzi wanaofuzu kujiunga na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi (TVET) kuanzia sasa yatafadhiliwa na serikali, akisema ahadi yake itatimia.
“Mimi si wazimu, na mimi si mlevi, na mimi si mjinga, I know what I am saying,” Ruto aliwajibu wenye mashaka juu ya mpango huo.
Amesema mswada tayari uko bungeni kuhakikisha ufanisi wa mpango huo, na kwamba wanafunzi wanaofuzu kujiunga na elimu ya juu kuanzia sasa watafadhiliwa kikamilifu na serikali.
“Nimesema juzi, kwenda mbele, tulitoa pale nyuma, 2022, mauniversities walikuwa wanafunga. Hawakuweza kuwalipa walimu, hawakuweza kulipa suppliers, walikuwa hata ile mshahara ya lecturers haikuwa inatosha. Nikabadilisha, tukatengeneza model mpya. Hiyo model imebadilisha mambo katika university,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia mafundistadi leo Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi
“Mimi nimesema sasa, tunapeleka hiyo model one more step forward. Na ndio nimesema, iko sheria bunge saa hizi ya Higher Education Loans Board Amendment Bill, ambayo sasa itatuwezesha kuhakikisha ya kwamba kila mtoto wa Kenya ambaye amekuwa placed kwa TVET ama University, tutahakikisha ya kwamba kuna funding ama kuna pesa ya kusomesha watoto wetu wote.”
Katika kile kinachoonekana kuwa habari njema hasa kwa wanafunzi kutoka familia maskini, Rais amesema nia ya serikali ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi kutoka familia kama hizo ambaye kiu yake ya masomo itakatizwa kwa sababu ya uhaba wa karo.
“Watoto wetu wa university na wale ambao wanaenda tertiary institutions, going forward, serikali ya Kenya itakuwa na funding model ya kuhakikisha hao watoto wote wanapata pesa ya kusoma na hakuna mtoto wa Kenya atakosa nafasi ya kusoma kwa sababu ya mambo ya kukosa pesa.”
Juzi Jumanne, Rais Ruto alitangaza kuwa masomo ya wanafunzi wanaofuzu kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi sasa watafadhiliwa kikamilifu kupitia mfumo mpya uliopendekezwa na serikali.
Ruto alisema hatua hiyo itahakikisha kila mwanafunzi anayejiunga na elimu ya juu anapata fursa ya kuendelezsa masomo yake bila kukabiliwa na changamoto za kifedha.
Aliongeza kuwa taifa hili linapaswa kuwekeza kwa elimu kwa sababu inampa kila mwanafunzi aliyefuzu fursa sawa ya ufanisi bila kujali familia alikotoka.