Bunge la Seneti litarejelea vikao vyake siku ya Jumanne alasiri wiki hii baada ya kukamilisha likizo yake ya miezi miwili.
Huo utakuwa mwanzo wa awamu ya nne ya vikao vya Bunge la Nne la Seneti vyenye shughuli nyingi.
Shughuli hizo ni pamoja na kubuniwa upya kwa kamati muhimu za bunge hilo.
Kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti ambaye pia ni Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot amesema masuala muhimu kuhusu fedha na sheria kama vile kupitishwa kwa taarifa ya sera ya bajeti ya mwaka 2025, yatapewa kipa umbele.
Bunge hilo pia litajadili kuhusu mswada wa ugavi wa mapato, mswada wa ugavi wa mapato kwa kaunti na mswada wa mapato ya ziada kwa serikali za kaunti pamoja na kuidhinisha mipangilio ya ugavi wa fedha.