Meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, ambaye awali aliahidi kumkamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu iwapo angetembelea jiji hilo, sasa amesema hana mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mamdani alisema badala yake anatoa wito kwa serikali ya Marekani kuchukua hatua kuhusu hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.
Kisheria, iwapo Netanyahu angeingia katika nchi mwanachama wa ICC, angeweza kukamatwa na kukabidhiwa mahakamani. Hata hivyo, Marekani si mwanachama wa ICC, hivyo haiwajibiki kutekeleza hati hiyo.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Netanyahu hatakamatwa kwa namna yoyote akiwa nchini Marekani.
Trump alisema Netanyahu anaendelea kupambana na Iran, ambayo aliituhumu kwa kuhusika na mauaji ya waandamanaji na wanajeshi wa Marekani.
Kauli hiyo ya Trump ilijibu mahojiano ambayo Mamdani alifanya na gazeti la The New York Times, ambapo alisema alikuwa akifanya mazungumzo na vyombo vya sheria kuhusu uwezekano wa kutekeleza hati ya ICC.
Hata hivyo, siku iliyofuata Mamdani alisema timu yake ya wanasheria imepitia njia zote zinazowezekana kisheria na kubaini kuwa ofisi ya meya haina mamlaka huru ya kutekeleza hati hiyo.
Aliongeza kuwa mamlaka hayo yako mikononi mwa serikali ya shirikisho la Marekani, na akaisihi Marekani ijiunge na ICC na kutekeleza hati hiyo ya kukamatwa.
Taarifa ya BBC