Bei ya mafuta yashuka nchini Tanzania

Imeshuka kwa Shilingi 92 kwa lita ya petroli, Shilingi 204 kwa lita ya dizeli na Shilingi 440 kwa lita ya mafuta ya taa, pesa za Tanzania.

Marion Bosire
1 Min Read

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania, EWURA imetangaza kupungua kwa bei ya mafuta nchini humo kufuatia mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia.

EWURA katika taarifa ilisema imechukua hatua hiyo ili kutekeleza majukumu kwa mujibu wa Sheria, baada ya kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia.

Mabadiliko hayo ya mara kwa mara yanatokana na vita inayoendelea eneo la Mashariki ya Kati ambapo kuna matumaini ya kuafikiwa kwa mkataba wa kusitisha vita.

Katika mwezi Agosti 2026, bei za mafuta nchini Tanzania zimeshuka kwa Shilingi 92 kwa lita ya petroli, Shilingi 204 kwa lita ya dizeli na Shilingi 440 kwa lita ya mafuta ya taa, pesa za Tanzania.

EWURA inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini humo zitakazotumika kuanzia Jumatano ya tarehe 05 Agosti 2026 saa 6:01 usiku.

Kwa mwezi Agosti 2026, bei za rejareja katika Mkoa wa Dar es Salaam ni 3898, 3978 na 4003 kwa kila lita ya Petroli, Dizeli na mafuta taa mtawalia.

Mkoani Tanga bei hizo za rejareja ni 3959, 4039 na 4065 kwa kila lita ya Petroli, Dizeli na mafuta taa mtawalia.

Share This Article