Gavana wa kaunti ya Kiambu, Kimani Wamatangi, amepuuza miito ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ya kutaka Kaunti ya Kiambu itenganishwe na eneo la Mlima Kenya au igawanywe kuwa kaunti mbili.
Kiongozi huyo alielezea kwamba mapendekezo hayo yanalenga kuleta mgawanyiko na yanasukumwa na maslahi ya kisiasa.
Wamatangi alikuwa akizungumza wakati wa mpango wa kuwezesha vyama vya ushirika vya waendesha bodaboda katika eneo bunge la Thika jana Alhamisi.
Alisema mapendekezo hayo yanaenezwa na viongozi ambao walishindwa kuleta miradi yenye manufaa ya maendeleo walipokuwa madarakani na sasa wameamua kutumia siasa za mgawanyiko.
Aliwataka wanaopigia debe mgawanyiko huo kuelezea rekodi yao ya maendeleo, akisema wakazi wa Kiambu wanajali zaidi utoaji wa huduma kuliko matamshi ya kisiasa.
Gavana huyo pia alipinga pendekezo la kutaka Kiambu itambuliwe kama eneo huru tofauti, akihoji msingi wa kikatiba wa pendekezo hilo.
Wamatangi alidai kuwa juhudi za kuleta mgawanyiko ndani ya Kiambu zinalenga kudhoofisha ushawishi wa kisiasa wa kaunti hiyo.
Aidha, Gavana huyo alitetea msimamo wake wa awali wa kuunga mkono mfumo wa ugavi wa mapato wa mtu mmoja, kura moja, shilingi moja, akisema amekuwa mstari wa mbele kupigania ugavi haki wa rasilimali za kitaifa kwa kaunti zenye idadi kubwa ya watu.