Matonya asema amewasamehe Wakenya

Hii ni baada yake kutangaza kuisha kwa kesi iliyomkabili ya ubakaji huko Mombasa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania wa mtindo wa Bongo Flava, Matonya ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya ubakaji katika mahakama ya Shanzu huko Mombasa, Kenya amesema kwamba amewasamehe Wakenya.

Huku akiwarejelea kama ndugu, Matonya alisema kwamba hawezi kutaka kuharibu uhusiano mzuri wa miaka kadhaa aliojenga na Wakenya.

“Ndugu zangu Wakenya, sipo tayari kupoteza upendo tulioutengeneza ndani ya miaka karibu 19, 20 au kumi na ushei kwa matatizo ya watu wachache,” alifafanua.

Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Sefu Shabani Ramadhan, anasema kwamba mahakama ya Shanzu imemwachilia huru na kumruhusu kuendelea na shughuli zake za kawaida za maisha.

“Mahakama za Kenya zimenipa nafasi nyingine ya kuniachia huru sasa rasmi na kwenda kuendelea na shughuli zangu,” alisema msanii huyo akielezea kwamba ana mengi ya kusema lakini hawezi.

Matonya alidaiwa kumdhulumu kingono mwanamke fulani mnamo tarehe 7 mwezi Aprili mwaka huu katika nyumba moja ya kukodisha katika mtaa wa Nyali, kaunti ya Mombasa.

Alikaa kizuizini kwa siku zipatazo 20 kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu shilingi laki 5, sarafu ya Kenya. Dhamana hiyo ilikuwana masharti kama vile kutosafiri nje ya Kenya bila idhini kabla ya kutamatika kwa kesi hiyo.

Kwa sababu hiyo, aliagizwa kuwasilisha stakabadhi zake mahakamani kama pasipoti ya usafiri na anasema sasa amekabidhiwa vitu hivyo na yuko huru.

Share This Article