Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dkt. Kizza Besigye na mshtakiwa mwenzake, Obeid Lutale, wanatarajiwa kurejea leo mbele ya Mahakama Kuu jijini Kampala.
Kikao hicho ni cha kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi ya utekelezaji wa haki za binadamu iliyofunguliwa dhidi ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Besigye anadai kuwa Jenerali Muhoozi alikiuka haki zake za kikatiba na kuhatarisha haki yake ya kusikilizwa kwa haki kwa kutoa hadharani kauli za kutishia kumuua au kumnyonga.
Wiki iliyopita, Jaji Emmanuel Baguma aliwapa wawili hao muda zaidi wa kutafuta mawakili wapya baada ya wakili wao mkuu, Erias Lukwago na Martha Karua kushindwa kuendelea kuwawakilisha kutokana na mazingira yaliyowakumba.
Lukwago alikamatwa kwa mashtaka tofauti na baadaye akalazwa katika Hospitali ya Mulago, huku Karua akifukuzwa kutoka Uganda.
Hata hivyo, katika barua waliyoielekeza kwa Jaji Baguma mwisho wa wiki iliyopita, Besigye na Lutale walikataa maelekezo ya kubadili mawakili wao wawili, wakisisitiza kuwa wana haki ya kikatiba ya kuchagua wawakilishi wao wa kisheria.
“Tunasisitiza kwamba hatujakata tamaa wala kuachana na haki yetu ya kuchagua mawakili wetu wenyewe,” barua hiyo inasema.