Trump adhihirisha imani ya kuafikiwa kwa makubaliano na Iran

Alisema kwamba Mlango wa Hormuz ungefunguliwa karibuni sana au Iran ingepigwa kwa nguvu sana.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump alisema kwamba Mlango Bahari wa Hormuz ungefunguliwa karibuni sana au Iran ingepigwa kwa nguvu sana.

Huku hayo yakijiri, bei za mafuta zimeshuka hadi kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha wiki tatu kutokana na matumaini ya kuafikiwa kwa makubaliano.

Rais wa Marekani alikuwa akizungumza na wanahabari baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na Waziri wa Fedha Scott Bessent kusema kuwa mazungumzo yalikuwa yamepiga hatua, jambo ambalo linaweza kuruhusu usafirishaji wa mizigo kupitia mlango huo kuanza tena baadaye wiki hii.

Bei ya pipa la mafuta ghafi aina ya Brent, ambayo ndiyo kipimo cha kimataifa cha bei za mafuta, ilishuka kwa karibu asilimia 5 hadi chini ya dola 80 kufuatia habari kwamba huenda usumbufu wa usambazaji wa mafuta ukapungua.

Hata hivyo, kushindikana kwa mazungumzo ya awali katika miezi ya hivi karibuni ili kupunguza mvutano wa mzozo kumesababisha soko la mafuta kubaki na mabadiliko makubwa ya bei, hali ambayo hatimaye huathiri madereva kupitia ongezeko la gharama za mafuta.

“Tunafanya mazungumzo mazuri sana,” Trump alisema akiwa katika ziara huko California, akisisitiza kuwa Iran ina hamu ya kuafikia makubaliano yatakayomaliza miezi kadhaa ya mzozo.

Afisi Kuu ya Jeshi la Marekani ilisema kuwa njia ya kusini kupitia Mlango wa Hormuz inaendelea kuwa huru na wazi kwa meli zote za kibiashara zinazotaka kupita.

Jumanne, sambamba na kushuka kwa bei ya mafuta ya Brent, bei ya mafuta ghafi ya Marekani aina ya West Texas Intermediate (WTI) pia ilishuka kwa zaidi ya asilimia 5 hadi dola 76 kwa pipa.

Bei za aina zote mbili za mafuta zilifikia kiwango cha chini zaidi tangu tarehe 13 Julai.

Share This Article