Mwanamume ahukumiwa maisha gerezani kwa kumdhulumu mtoto wake kimapenzi

Mshtakiwa huyo awali alikanusha kutekeleza kosa hilo, na kusababisha upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi 6.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwanamume ahukumiwa maisha gerezani kwa kumdhulumu mtoto wake kimapenzi.

Mahakama moja ya Kisumu imemhukumu mwanamume kifungo cha maisha gerezani, kwa kumdhulumu mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 10 kimapenzi.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Lele Lucas Ikapolon, alimpata mshtakiwa huyo na kosa hilo kinyume na sheria za kukabiliana na makosa ya ngono sehemu ya 8(1) inayoambatana na sehemu ya 8(2) nambari 3 ya mwaka 2006.

Mahakama  ilifahamishwa kuwa kati ya tarehe tofauti mwezi Jamuari mwaka 2026 na tarehe 18 mwezi Mei mwaka 2026, katika kaunti ndogo ya Kisumu, mshtakiwa huyo alimdhulumu mtoto huyo na kumsababishia majeraha mabaya.

Mshtakiwa huyo awali alikanusha kutekeleza kosa hilo, na kusababisha upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi 6 mahakamani, akiwemo afisa wa afya aliyemchunguza mtoto huyo kiafya.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mshtakiwa huyo aliwasili nyumbani tarehe 18 mwezi Mei mwaka 2026 akiwa mlevi, aliingia chumbani kwa msichana huyo akiwa uchi na kumdhulumu huku akimpiga na hatimaye kuchoma nguo zake.

Msichana huyo alitoroka kwao na kutafuta hifadhi kwa jirani. Siku iliyofuatia alienda shuleni na kuwaarifu walimu. Mwalimu Mkuu alimfahamisha afisa wa watoto aliyempeleka msichana huyo hospitalini kwa uchunguzi.

“Upande wa mashtaka umethibitisha kuwa mtoto huyo alidhulumiwa,” alisema hakimu Ikapolon.

TAGGED:
Share This Article