Wasafiri wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA watashuhudia mabadiliko makubwa huku serikali ikiimarisha udhibiti wa uwanja huo kwa lengo la kuongeza kasi na ufanisi wa huduma.
Miongoni mwa hatua zinazotekelezwa ni kuanzishwa kwa Huduma ya Kielektroniki ya Habari za Vituo, ATIS, mfumo unaolenga kuboresha utambuzi na usimamizi wa ndege zinazoingia na kutoka.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya, KAA pia inapanga kuboresha mpangilio wa shughuli za vituo, ikiwemo kuweka mfumo wa pamoja wa huduma za kuingia kwa abiria na ukaguzi wa usalama, pamoja na kutenganisha maeneo ya wanaowasili na wanaoondoka.
Ujenzi wa kituo kipya cha abiria tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 54 na kinatarajiwa kuongeza uwezo wa kuhudumia takribani abiria milioni 10 kwa mwaka.
Serikali pia inaendeleza mfumo ulioimarishwa wa usajili wa wasafiri huku miundombinu ya kudhibiti data ikitarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya mwezi mmoja.
Wakati huo huo, KAA imeanza kukaza kamba dhidi ya ukiukaji wa taratibu za mizigo.
Wasafiri wameonywa dhidi ya kuunganisha mizigo yao na ya abiria wengine, huku mashirika ya ndege yakikabiliwa na hatua za kisheria iwapo yatasafirisha mizigo nje ya njia zilizoidhinishwa.
Mabadiliko hayo ni sehemu ya mpango wa kisasa wa JKIA wa thamani ya shilingi bilioni 154.2, unaolenga kuongeza uwezo wa uwanja huo kutoka takribani abiria milioni nane hadi milioni 12 kwa mwaka.