Watu 13 wanahofiwa kufariki na wengine 22 kujeruhiwa kwenye shambulizi la droni katika jimbo la Kordofan Kaskazini mwa Sudan.
Kulingana na kundi moja la madaktari, shambulizi hilo lilitekelezwa siku ya Jumanne na lililenga makazi ya raia katika mji wa Um Rawaba.
Kupitia kwa taarifa, Mtandao wa Madaktari nchini Sudan ulitaja shambulizi hilo kama mauaji mapya ya halaiki, huku ukinyonshea kidole cha lawama kundi la wapiganaji la Rapid Support Forces (RSF) kwa kulitekeleza.
Walioshuhudia walisema droni hiyo ilirusha makombora matatu kwenye jumba la makazi ambapo raia walikuwa wamekusanyika, pamoja na majengo mengine ya utawala.
Mashambulizi hayo yalisababisha hofu miongoni mwa wananchi waliotorokea maeneo salama. Waliojeruhiwa, kulingana na mtandao huo wa madaktari, walipelekwa katika hospitali ya Um Rawaba kwa matibabu.
Jimbo la Kordofan Kaskazini limeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya droni na operesheni za kijeshi huku vita vikiendelea kati ya vikosi vya usalama na wapiganaji wa RSF.
Vita hivyo vimesababisha maafa ya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kuachwa bila makazi.